Saturday 5 December 2015

Ndugu Wasamaria wema,

Tunapenda  kutumia fursa hii kuwapa updates kuhusu dada Joyce Mwambepo, mkaazi wa Sinde jijini Mbeya mwenye umri wa miaka 27 ambaye anaishi na bibi yake mwenye umri wa miaka 80 pamoja na mwanaye mwenye umri wa miaka 4.

Kwa bahati mbaya mwezi April mwaka jana dada huyu alipata ajali ya kugongwa na gari ambalo dereva wake hakusimama kumsaidia. Ila kwa msaada wa wasamaria wema alipelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mbeya ambako inasemekana alikaa kwa miezi mitatu bila kupata matibabu kwa kukosa fedha. Katika uchunguzi wa awali ilibainika kuwa Joyce amevunjika miguu yote miwili,  hivyo akahamishiwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili ambako pia baada ya kukaa kwa miezi kadhaa alirejeshwa Mbeya baada ya kukosa pesa za matibabu.

Baada ya mwanahabari Deo Kakuru wa Mbeya kumgundua na kufanya juhudi za kutoa taarifa za dada Joyce katika mitandao mbalimbali, wasamaria wengi  wa ndani na nje ya nchi  wakaguswa na kuchangia. Mungu mkubwa, kiasi kilichopatikana (kiasi cha 3.2m/-) kimewezesha dada Joyce kupelekwa Dar es salaam toka Mbeya kwa ndege ya Fast Jet Alhamisi iliyopita na moja kwa moja kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kupokelewa katika kitengo cha MOI na kupatiwa kitanda katika wodi mpya ijulikanayo kama Wodi ya Magufuli, ghorofa ya tatu chumba namba mbili.

Cha kufurahisha ni kwamba Joyce aliweza kukaa kwenye kiti cha kusukumwa na hata kwenye ndege aliketi kama kawaida, zoezi ambalo hata yeye anasema limemsaidia kwani kwa mara ya kwanza hivi sasa ganzi miguuni inapotea taratibu na ukimgusa anahisi mguso tofauti na ilivyokuwa awali.
Daktari bingwa ameshaonana naye na kumpa matumaini ya kupona, hasa sehemu ya chini ya uti wa mgongo wake ambao inasemekana una matatizo yaliyopelekea kubana  mishipa ya fahamu na kufanya miguu ipooze. Zoezi linalosubiriwa kwa sasa ni kupatiwa vipimo vya MRI ili kubaini kiufasaha tatizo lake na hatimaye kupatiwa matibabu. Zoezi hili linatarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Mpiganaji Deo Kakuru amesharejea Mbeya na kijiti cha kumwangalia dada Joyce amekabidhiwa Ankal ambaye anaomba Wasamaria wema waendelee kumuombea na kumsaidia kwa hali na mali dada huyu ambaye ni yatima.
Kwa bahati njema Ankal alikutana na kuongea na Msamaria mwingine aitwaye Mama Rozi ambaye  anamuuguza mama yake mzazi aliyelazwa  wodi moja na dada Joyce. Msamaria huyu amekubali kumsaidia dada Joyce kwa chakula na pia kumsaidia usafi maana hapo kitandani hawezi kuondoka.
Mungu kweli ni mkubwa. Dada Joyce anatabasamu na kuongea vizuri tu. Anatoa shukurani sana kwa wote waliomsaidia na wanaoendelea kumsaidia. Anasema hana cha kuwalipa ila kusema ASANTE SANA na anamwomba Mola Muumba awazidishie pale patapopungua. Ameomba anayeweza kumtembelea atafurahi sana maana hana ndugu hapa Dar es salaam.Pia anawashukuru sana madaktari waliomhudumia vyema katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ambao amesema hatowasahau kwa msaada wao.
 Ankal amejitolea kuendelea kusaidia uratibu wa kufanikisha matibabu ya dada Joyce. Hivyo unaweza kuwasiliana naye kwa email issamichuzi@gmail.com ama whatsapp namba+255 754 271266 kwa jina la Ankal.
AU mratibu-mwenza  Deo Kakuru Msimu
Pia unaweza kuwasiliana moja kwa moja na dada Joyce kwa namba

 Mpiganaji Deo Kakuru akiwa na dada Joyce ndani ya FastJet wakitoka Mbeya keuelekea Dar es salaam 
 Dada Joyce akiwa ameketi kwa utulivu kwenye siti yake ndani ya ndege
 Mpiganaji Deo Kkuru akiwa na dada Joyce mara baada ya kuwasili  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es salaam
 Msamaria mwema Mama Rozi akimhudumia dada Joyce akiwa kitandani kwake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kitengo cha mifupa cha MOI katika wodi ijulikanayo kama Wodi ya Magufuli ghorofa ya tatu

Dada Joyce akiwa wodini Moi