Wednesday 9 December 2015

IMG_6503 Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (wa pili kulia) na ujumbe wake aliombatana nao Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini, Dkt. Natalia Kanem (wa pili kushoto) pamoja na Ofisa wa Mambo ya Nje kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maulidah Hassan (kushoto) kabla ya kuelekea kambi ya Nyarugusu walipita ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Gerald Guninita kumsalimia pamoja na kusaini kitabu cha wageni. (Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog). Na Mwandishi Wetu, Kigoma JUMUIYA ya Kimataifa imekumbushwa kuisaidia Tanzania katika kuhudumia wakimbizi kutoka Burundi na Kongo ambao wanaishi katika kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma. Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez wakati akizungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kukamilisha ziara yake mkoani Kigoma. Alisema kwamba serikali ya Tanzania kwa miaka mingi imekuwa na moyo wa huruma wa kusaidia majirani zake kwa kuhifadhi wakimbizi na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuona hilo na kusaidia Tanzania kufanikisha hifadhi ya wakimbizi. Alisema Umoja wa Mataifa umekuwa ukishuhudia namna ambavyo serikali ya Tanzania inahudumia wakimbizi na kuridhika na hata pale ilipowapatia haki za kuwa Watanzania kwa kuwapa uraia na pia kusaidia kuwarejesha makwao wakati hali ilipokuwa njema. Hata hivyo amesema kwa sasa hali ya Burundi na Kongo si njema na hivyo Watanzania kupata tena kazi yakuhifadhi wakimbizi. Alisema Tanzania kwa huruma yake imetoa ardhi zaidi ili kupunguza msongamano katika kambi ya Nyarugusu na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kusaidia kukamilisha makazi hayo mapema kabla ya mvua za masika ili wananchi hao waweze kuishi kwa amani. IMG_6505 Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Gerald Guninita akimsikiliza kwa makini Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (hayupo pichani) alipomtembelea ofisini kwake kabla ya kuelekea kambi ya Wakimbizi Nyarugusu. Alisema kambi ya Nyarugusu ni ya tatu kwa ukubwa duniani na inahifadhi zaidi ya wakimbizi 150,000 wakiwemo watoto na wanawake na wanahitaji huduma za shule, afya, maji na mengine. Aidha wanahitaji nishati na hali hiyo haiwezi kuwezeshwa na serikali ya Tanzania pekee kwani watakuwa wakielemewa na huruma yake na moyo wa upendo kwa majirani zake. “Dunia ikumbuke wema wa watanzania kwa miaka yote hii, na isaidie kuweka sawa hali ya kambi hiyo ili huduma zote muhimu za wananchi zipatikane” alisema mratibu huyo. Akizungumza kuhusu wajibu wa Umoja wa Mataifa, alisema mashirika yake yamekuwa yakishirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kwamba wanatoa huduma kwa wakimbizi hao na kutaka wadau duniani kusaidia mashirika hayo na serikali ya Tanzania kufanikisha mahitaji muhimu kwa wakimbizi hao hadi hali itakapokuwa shwari katika nchi zao na kurejea kuishi makwao. Tanzania imetoa maeneo matatu zaidi ya kupunguza msongamano katika kambi ya Nyarugusu na maeneo hayo yanahitaji huduma za msingi kama barabara, maji, vituo vya afya na shule. Katika ziara hiyo ambayo aliambatana na Ofisa wa Mambo ya Nje kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maulidah Hassan, pamoja na kukagua maendeleo ya kambi ya Nyarugusu pia walikagua miradi inayofadhiliwa na Shirika la Kazi Duniani ILO na ile ya Shirika la Mpango wa idadi watu duniani UNFPA. ILO Kigoma inaendesha mafunzo ya ujasirimali kwa vijana kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri wenyewe na kuhudumia familia zao kwa kuziwezesha kupata huduma bora za elimu na afya kutokana na kipato chao. IMG_6515 Katika msafara huo walikuwepo maafisa kutoka Shirika la linalohudumia Wakimbizi (UNHCR) ofisi ya Kasulu mkoani Kigoma (walioipa mgongo kamera). Alisema kwamba amefurahishwa na mradi huo ambao unawawezesha vijana kutambua fursa mbalimbali zilizopo na kuzitumia vyema kufanikisha maendeleo ya familia zao. “Naona uwezekano wa vijana hawa kujiajiri na kuziwezesha familia zao kuondokana na tatizo la kipato.. elimu hii inaweza kutanzua mambo mengi na kuondoa changamoto nyingine zinazoambatana na kukosa kipato” alisema mratibu huyo. Mkoa wa Kigoma una mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa yakifanya kazi mbalimbali za maendeleo na za kutoa huduma za kibinadamu kwa wakimbizi. Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yanayotekeleza miradi mbalimbali mkoani Kigoma ni pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Shirika la Afya Duniani ( WHO), Shirika la Mpango wa Uzazi (UNFPA), Shirika la Kazi la Kimataifa ( ILO), Shirika la Kuhudumia Watoto ( UNICEF), Shirika la Kuhudumia Wahamiaji ( IOM), Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la maendeleo (UNDP). Akizungumza Afisa anayeshughulikia Ustawi na Usalama UNHCR, Kasulu, Bi. Zenobia Mushi, alisema shirika lake litaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania na ya mkoa wa Kigoma katika kuhudumia wakimbizi kwa kuhakikisha kwamba mahitaji yao ya msingi yanapatikana. Naye Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Kanali Mstaafu Issa Machibya alishukuru Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa tayari kusaidia mkoa wake. “ Tunashukuru kwa mambo yanayofanywa na Umoja wa Mataifa katika dhima nzima ya ushirikiano katika kuhakikisha kwamba pengo la maskini na matajiri linazibwa na umaskini unaondolewa katika mkoa wa Kigoma.” IMG_6520 Ofisa wa Mambo ya Nje kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maulidah Hassan akipiga picha kwenye bango linaloonyesha Serikali zinazofadhili misaada kwa Wakimbizi nchini Tanzania lililopo katika ofisi za UNHCR Kasulu. Naye Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Gerald Guninita akizungumza kuhusu hali ya kambi ya Nyarugusu alisema kwamba hali ya kambi si nzuri na wakati msimu wa masika ukikaribia ni vyema Jumuiya ya Kimataifa ikaharakisha kukamilisha miundombinu ili kupunguza msongamano Nyarugusu. Serikali imetoa maeneo mengine ya Nduta yaliyoko Kibondo na na Ntendeli, Kakonko kwa ajili ya kupunguza uwingi wa watu katika kambi hiyo. DC huyo pia alisema kwamba kuna uharibifu mkubwa wa mazingira na lazima wadau wote washirikiane kuhakikisha kwamba mazingira yanaboreshwa pamoja na kupokea wakimbizi na kuwapa makazi. Alisema kambi hiyo ilipangwa kuwa na watu elfu 50 kwa miaka ya 1996 lakini sasa inaweka wakimbizi wengi zaidi. Aidha alisema kwamba pamoja na kupokea wakimbizi hao, inaonekana baadhi yao wameingia kufanya uhalifu na kuomba wakimbizi kushirikiana na polisi kuwataja wahalifu hao ili wadhibitiwe. IMG_6551 Kuwepo kwa kundi kubwa la wakimbizi kunasababisha uharibifu wa mazingira kama inavyoonekana pichani wakimbizi wakitoka kukata kuni kwenye misitu iliyopo karibu na kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Aidha katika mazungumzo ya shukurani kwa namna serikali ya Kigoma inavyotoa ushirikiano kwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa katika miradi ya maendeleo na misaada kwa wananchi na kwa wakimbizi, Mwakilishi wa Shirika la mpango wa idadi ya watu duniani (UNFPA), Dkt. Natalia Kanem alisema kwamba kumekuwepo na mafanikio mengi kutokana na ushirikiano huo. Alisema anachokiona yeye anaona hali ya baadae ya taifa la Tanzania kuwa bora zaidi kutokana na kuwapo kwa ushirikiano mzuri kati ya serikali, mashirika ya umma na kundi kubwa la vijana ambalo kwa sasa linapokea elimu mbalimbali kwa manufaa yao na ya baadae. “Taifa la Tanzania nusu yake ni vijana na sehemu kubwa ni chini yake, taifa hili lina hali njema kabisa ya siku za usoni kutokana na ushirikiano wenye lengo la kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na wengi” alisema Kanem. Anasema kwa kuangalia program zilizopo zinazotekelezwa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa na serikali anaona mafanikio ya mafunzo ya ujasiriamali na pia elimu inayotolewa kwa watu kwa malengo ya kufanikisha maendeleo. IMG_7365 Alisema UNFPA imefurahishwa sana namna mafunzo yanavyoendeshwa kwa vijana mafunzo ambayo yanaleta mshikamano wa pekee katika kufanikisha ustawi wa jamii na taifa kwa jumla. Aidha alifurahi kuona kwamba wanawake wanashiriki katika kutoa elimu hivyo kuingiza sauti katika mafanikio ya jamii na uongezaji wa uelewa miongoni mwa jamii. Mratibu huyo Mkazi wa UN Tanzania, Alvaro Rodriguez na timu yake wamerejea Dar es Salaam baada ya ziara ndefu kuangalia miradi ya Umoja wa Mataifa inavyoleta tija na ufanisi wa maisha katika jamii. Mratibu huyo alitembelea mikoa ya Manyara, Singida, Tabora na Kigoma. Katika ziara yake alioneshwa kufurahishwa na miradi hiyo inavyobadili jamii husika na kusema kwamba umoja huo utaendelea kufadhili miradi ya maendeleo nchini Tanzania. IMG_6558 IMG_6601 Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu B, Fredrick Nisajile (kulia) akielezea changamoto mbalimbali zinazowakabili kambini hapo kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez (wa pili kulia) na ujumbe wake aliombatana nao Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini, Dkt. Natalia Kanem (wa pili kushoto) pamoja na Ofisa wa Mambo ya Nje kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maulidah Hassan (kushoto) kabla ya kutembelea makazi ya wakimbizi hao. IMG_6608 Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini, Dkt. Natalia Kanem (kulia) na Ofisa wa Mambo ya Nje kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maulidah Hassan wakirekodi mambo muhimu wakati wa kupokea taarifa ya maendeleo ya kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu kutoka kwa Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu B, Fredrick Nisajile (hayupo pichani). IMG_6624 Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini, Dkt. Natalia Kanem akizungumza jambo kwenye mkutano wa kupokea taarifa ya kambi hiyo. IMG_6632 Kutoka kushoto ni Afisa mahusiano wa UNHCR, Ofisi ya Kasulu, Agnes Mwangoka, Mshauri na Mtaalum wa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa Tanzania, Hoyce Temu, Mwandishi wa Habari, Prosper Kwigize pamoja na Ofisa wa Mambo ya Nje kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maulidah Hassan wakielekea kwenye kambi za Wakimbizi baada ya kupokea taarifa. IMG_6664 Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini, Dkt. Natalia Kanem wakikagua ndani ya mahema wanakoishi Wakimbizi wapya wanaoendelea kuwasili katika kambi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma. IMG_6668 Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini, Dkt. Natalia Kanem wakiuliza jambo kwa Ofisa Mtafiti Mshirikishi wa ofisi za UNHCR, Kasulu, Mariam Khokhar walipotembelea ndani ya mahema wanakoishi Wakimbizi wapya wanaoendelea kuwasili katika kambi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu B, Fredrick Nisajile. IMG_6659 Eneo la mahema ya kulalia familia za Wakimbizi wapya wanaoendelea kuwasili katika kambi ya Nyarugusu. IMG_6661 Mmoja wa Wakimbizi akiwa na mwanae nje ya chumba chake na mwanae katika kambi ya Nyarugusu. IMG_6682 Kuni zikitumika kupikia chungu cha Maharage kambini hapo. IMG_6703 Mtoto ambaye jina lake halikuweza kupatikana kiurahisi akikoleza moto ulioonekana kufifia wakati akijiandalia chakula chake cha mchana kama alivyonaswa na kamera yetu. IMG_6710 Moja ya familia ya Wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu wakiangalia msafara wa Mkuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini uliotembelea kambini hapo mwishoni mwa juma. IMG_6725 Ofisa wa Mambo ya Nje kutoka Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maulidah Hassan akipozi na moja ya familia katika kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu. IMG_6732 Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez akisalimiana na Rais wa kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, Bi. Abilola Angelique wakati wa ziara yake ya kutembelea kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma.Kwa matukio zaidi ya picha bofya link hii