Thursday 8 October 2015

 Mkutano ukiwa unaendelea huku wanakijiji wakifuatilia 
 Mmoja wa wanakijiji akiongea wakati wa Shughuli hiyo ya kukabidhi hati
 Mgeni rasmi wa hafla hizo katibu tawala wa Wilaya ya Hanang’ John Gabriel akizungumza kabla ya kukabidhi rasmi vyeti.
 Mwenyekiti wa kijiji cha Mreru James Gejaru akipokea hati ya hakimiliki ya ardhi ya kimila ya kijiji chake.
 Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Dirma Agustino Majawa akipokea hati ya hakimiliki ya ardhi ya kimila ya kijiji chake
 hati ya hatimiliki ya kimila
  Mwanakijiji akipokea hati ya hakimiliki ya ardhi yake
 Mwanakijiji akipokea hati ya hakimiliki ya ardhi yake
 Wananchi na viongozi wa Serikali ya kijiji  wakipitia kwa makini hati za hakimiliki za kimila za ardhi.
Sherehe zilipambwa na ngoma ya wa-Barbaig

Na mwandishi wetu
Wenyekiti wa vijiji vinne vya wilaya ya Hanang’ wamepokea hati za hakimiliki za kimila za ardhi ya vijiji vyao baada ya kuwa vimepimwa na wao kupewa mafunzo ya matumizi bora ya ardhi kwa ufadhili uliotolewa na shirika la Oxfam kupitia shirika la Ujamaa Community Resource Team - UCRT.

Vijiji hivyo vya Mureru, Ming'enyi, Dirma na Gehando vimekabidhiwa hati hizo na katibu tawala wa Wilaya ya Hanang’ John Gabriel aliyemuwakilisha mkuu wa wilaya hiyo katika hafla fupi iliyofanyika katika kijiji cha Mureru na kuhudhuriwa na wakazi zaidi ya 100 kutoka katika vijiji hivyo vinne.

Akiongea kwa niaba ya wenyeviti wa vijiji hivyo vinne, Mbisha Gicharoda ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Ming’enyi aliyashukuru mashirika ya Oxfam na UCRT kwa kuwapatia elimu ya matumizi bora ya ardhi na kuwasaidia kupata hati za hakimiliki za ardhi ya vijiji. "Sisi kama wafugaji tulikua hatujui thamani ya ardhi yetu, sasa tumeamka na kujua haki zetu na manufaa ya kuwa na cheti cha umiliki wa ardhi", aliongezea.

Aidha mwenyekiti huyo alisema vijiji vyao kupata hati za hakimiliki za ardhi itawasaidia kuwa na eneo la pamoja la malisho na itawasaidia kuwa na nguvu zaidi ya kuilinda ardhi yao na kuisimamia vyema hali ambayo itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi.

Katika hatua nyingine, afisa ardhi wa wilaya ya Hanang' Bi Eveline Mirai aliyashukuru mashirika ya Oxfam na UCRT kwa kuwasaidia wakina mama wajane nao kupata hati za hakimiliki za maeneo yao iliyoenda sambamba na kusaidia vijiji hivyo vinne kupata hati za vijiji.

Eveline alitoa wito kwa wananchi kuheshimu mipaka inayowekwa kisheria kwa sababu mipaka hiyo inawekwa kwa gharama na wananchi wenyewe wanakuwa wameikubali. “Mtakapoheshimu mipaka, hatutakua na migogoro ya ardhi” na akawataka wananchi wenye maeneo yao kuhakikisha wanapata hati za hakimiliki za maeneo yao ili wayamiliki kisheria.

Naye meneja wa program ya ufugaji kutoka Oxfam Laurent Wambura aliwapongeza wakazi wa vijiji hivyo vinne pamoja na wananchi mmoja mmoja ambao nao walipokea hati zao siku hiyo. "Ukilinda maeneo ya wafugaji maana yake ni kwamba umewahakikishia maisha yao, tunapenda kuona haki za wafugaji zinapatikana" aliongezea.

Wambura aliishukuru serikali hususani Halmashauri ya wilaya ya Hanang’ kwa ushirikiano mkubwa ambao wameutoa kufanikisha zoezi hili na akatumia fursa hiyo kutoa wito kwa serikali kushirikisha mashirika na wadau mbalimbali wa maendeleo wakati wa ugawaji wa maeneo ya ardhi za vijiji kwani wanapogawa vijiji wakati mchakato wa upimaji unaendelea ni hasara kwa mashirika hayo kwani aidha yanalazimika kuanza kazi upya au kushindwa kwa sababu tayari fedha zinakuwa zimetumika na tatizo kwa wananchi linakuwa halijatatuliwa.

Naye Makko Sinandei Mratibu wa Miradi wa shirika la UCRT alisema wamekutana na changamoto za migogoro ya mipaka katika vijiji ambayo inazuia kushindwa kupima mipaka katika vijiji husika.

Changamoto nyingine ni pamoja na udhaifu katika uongozi wa serikali ya vijiji ambazo huchelewesha mipango lakini pia kuchelewa kupata ripoti ya matumizi ya ardhi kutoka wizarani nayo ni changamoto.

Naye Mgeni rasmi wa hafla hizo katibu tawala wa Wilaya ya Hanang’ John Gabriel aliyemuwakilisha mkuu wa wilaya hiyo, alipozungumza kabla ya kukabidhi rasmi vyeti hivyo alizitaja faida za kumiliki ardhi kisheria kuwa ni pamoja na ardhi ile huwezi kupokonywa na mtu kirahisi, utajua mipaka ya eneo lako ambayo huwezi kuingiliwa na mtu na vilevile inaweza kuwa rasilimali baadaye ukapata fedha kukuwezesha kufanya vitu vingine zaidi.

Akitolea mfano, John alisema "Mara nyingi wakina mama huwa wanakosa haki yao pale mume anapofariki, huwa ananyanganywa mali yote ikiwa ni pamoja na ardhi wakati anaachiwa watoto awatunze, lakini wanapokuwa na hati za hakimiliki hakuna mtu anayeweza kuwapokonya kirahisi."