Saturday 31 October 2015

TULINDE AMANI TUNAPOENDELEA KUPOKEA MATOKEO YA UCHAGUZI MKUU

Ndugu watanzania wenzetu, tunapenda kuwapongeza kwa kumaliza mchakato wa kampeni za vyama vya siasa na wagombea  kwa amani na utulivu. Vile vile tunawapongeza kwa kupiga kura kwa kwa amani na utulivu, kwani pamoja na kujitokeza kwa wingi tulipiga kura kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ukiachilia mbali kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza katika zoezi hilo. 
Ndugu watanzania wenzetu,  tangu juzi jumapili 25 Oktoba tulianza kupokea matokeo. Hiyo ni hatua muhimu sana kwa taifa letu, demokrasia yetu na amani ya nchi yetu. Wote tutakubaliana kwamba nchi nyingi za kiafrika zimeingia katika machafuko ya kisiasa na kuvuruga amani ya nchi hizo katika kipindi cha kupokea matokeo. 
Nchi za Ivory Cost iliingia katika mgogoro wa kisiasa kwa wakati wa kupokea matokeo, ikaingia katika mapigano  ya wenyewe kwa wenyewe maelfu ya wananchi walipoteza maisha, wengine wakijeruhiwa vibaya na wengi wakiyakimbia makazi yao. 
Mwaka 2007, Nchi jirani ya kenya nayo ilingia katika mgogoro wa kupokea matokeo na hivyo kusababisha machafuko, watu zaidi ya elfu moja walipoteza maisha, wengi wakiachwa walemavu na maelfu wakiyakimbia makazi yao. 
Sisi Global Peace Foundation Tanzania, tunaona mwenendo wa kupokea matokeo ukianza kuingia dosari, kwa baadhi ya wagombea na wafuasi wa wagombea kujitangazia matokeo. Ambao kwa Mujibu ka sheria ya uchaguzi ni kinyume, ni kuvunja kanuni kwani chombo chenye dhamana ya kutangaza matokeo ni Tume ya Taifa ya uchaguzi pekee. 
Kwa sababu hiyo, tumeona tuwakumbushe wanasiasa na viongozi wa vyama vya siasa kuwa wakati huu wanapaswa kuwa watulivu na waangalifu pindi wanapotoa matamko. Kwa kufanya hivyo watakuwa wamewasaidia wafuasi wao kuwa watulivu na hatimaye kutuvusha katika hatua hii tukiwa na amani na utulivu. 
Tunaisihi tume ya uchaguzi ya Taifa NEC, na ile ya Zanzibar ZEC, kuharakisha mchakato wa kutangaza matokeo pindi yanapopatikana na kujumlishwa ili kuepusha minong'ono na hisia hasi zinazoweza kupandikizwa kwa wapiga kura na wananchi na baadaye kusababisha machafuko. 
Tunakiri kuwa pamoja na kuwapo migogoro ya hapa na pale, kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo kama huko Unguja Zanzibar, baadhi ya maeneo ya Mbeya, Dar es Salaam na Lindi. Bado jeshi la polisi limeendelea kufanya kazi zake kwa weledi. Hata hivyo tunakisii chombo hicho kuwa waangalifu zaidi katika kipindi hiki adhimu kwani matumizi ya nguvu zilizopitiliza yanaweza kuchochea uvunjifu wa amani. 
Tunawakumbusha watanzania wenzetu mashabiki wa vyama vya siasa , wapiga kura na vyama vya siasa wajiandae kupokea matokeo ya aina yeyote. kwani misingi ya kidemokrasia inatutaka kuchagua na yule aliyepata kura nyingi ndiyo anakuwa mshindi. 
Na mwisho ni kwa wanahabari na vyombo vya habari nyie mnabeba dhamana kubwa kwa taifa hili katika wakati huu muhimu kwa taifa letu. Namna mtakavyotoa taarifa kwa watanzania ndiyo itakayo amua mustakabali wa amani na utulivu wa taifa hili. Mnalo jukumu na wajibu mahususi katika kuhakikisha kuwa nchi hii inabaki salama, inabaki na umoja na mshikamano, inabaki na utulivu. Toeni habari kwa kulingana na matakwa ya taaluma yenu muhimu. 
Waswahili husema, sindano ya daktari huponya na kuua na kalamu ya mwandishi hujenga ama kubomoa. Kama ilivyo daktari mwema, mwenye maadili huchagua kuponya na mwandishi makini atachagua kujenga jamii yenye amani, utulivu na mshikamano kwa kutambua kuwa bila amani hakuna maendeleo. 
Tunasimamia msemo wa watanzania uliopata umaarufu katika wakati huu wa uchaguzi kuwa KUNA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI . Asanteni, Mungu ibariki Africa, Mungu ibariki Tanzania

Tafadhali bonyeza hapa chini kusikiliza wimbo maalumu wa kuhamasisha Amani ulioimbwa na Barnaba Boy