Wednesday 7 October 2015


Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Ujenzi, Segolena Francis (kulia), akizungumza na wanahabari Dar es Salaam leo asubuhi wakati akimkaribisha  Mkurugenzi wa Barabara wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Ven Ndyamkama (kushoto), kuzungumza na waandishi wa habari  kuhusu mafanikio ya serikali katika sekta ya ujenzi kwa kipindi cha  miaka 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2015.

Mkurugenzi wa Barabara wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Ven Ndyamkama (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, kuhusu mafanikio ya serikali katika sekta ya ujenzi kwa kipindi cha  miaka 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2015. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, Segolena Francis.
Hapa mkutano ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale

WIZARA ya Ujenzi imesema itashirikiana na Sekta Binafsi
(PPP) kuhakikisha kuwa baadhi ya miradi ya barabara inajengwa na sekta hiyo ili
kukamilisha miundombinu ya usafiri nchini.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Barabara katika Wizara hiyo
Mhandisi Ven Ndyamukama wakati akizungumza na waandishi wa habari leo katika
Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.

Alisema mfano wa mradi wa ushirikiano wa Serikali na PPP ni
barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze ambayo itakuwa na njia sita unatarajiwa
kuanza hivi karibuni.

Alisema lengo la Serikali kushirikiana na sekta binafsi ni
kuhakikisha kuwa miradi mingi inakamilika kwa wakati ambapo kwa kipindi cha
miaka 10 ya Serikali ya awamu ya nne wamekamilisha ujenzi wa kilometa 5,568 za
lami zilizogharimu sh. bilioni 4,090 kati kilometa 17,762 ambazo zilitarajiwa
kujengwa.

"Tumejipanga kushirikiana na sekta binafsi katika
utekelezaji wa miradi mingi hapa nchini lakini kwa kuanza ni huu wa Dar es
Salaam hadi Chalinze unaotarajiwa kuanza hivi karibuni," alisema.


Pia alisema kilometa 3,873 zinaendelea kujengwa kwa kiwango
cha lami kwa gharama ya jumla ya sh.bilioni 4,533 na barabara zenye urefu wa
kilometa 4,965 zimefanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa gharama ya
shilingi bilioni 29.257 ambapo Serikali inatafuta fedha za ujenzi wa lami.