Saturday 25 April 2015

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS, UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI WA MIRADI,
 GHOR. 1, JENGO LA AIRTEL,
MAKUTANO YA BARABARA ZA
A.H. MWINYI/KAWAWA,
 P.0. Box 3815,
 DAR ES SALAAM.
 
Simu:            +255 22 292 6032
Nukushi:     +255 22 292 6033
E-mail:         info@pdb.go.tz


 




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 MAABARA YA BRN KUCHAMBUA CHANGAMOTO YA MASOKO KATIKA KILIMO
Jumatatu, April 21, April, 2015: Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), imealika wataalamu wa kilimo ili kuchambua na kutoa mapendekezo juu ya namna bora nchi inavyoweza kutatua changamoto ya masoko kwa wakulima. Ili kufikia lengo hilo, maabara ndogo ya siku tano imeandaliwa ili kutathmini mifumo ya sasa ya masoko kwa mazao ya mahindi na mpunga.  
Akifungua maabara hiyo jijini Dar es Salaam, Jumatatu, Mtendaji Mkuu wa PDB, Bw. Omari Issa amewataka wadau wote husika kufanya kazi hiyo kwa pamoja katika kuleta majibu yanayolenga mikakati ya muda mfupi na mrefu ili kuwapatia nafuu wakulima.  
Alisisitiza kuwa nidhamu ya kiutendaji ya BRN inawataka wadau wa sekta za umma na binafsi kufanyakazi kwa pamoja ili kutatua changamoto zinazozikabili sekta muhimu; ikiwemo ya kilimo na kuongeza kuwa majibu ya changamoto za masoko kwa wakulima yatakoka kwenye pande pande hizo mbili. Maabara hiyo ndogo inajumuisha wawakilishi 50 kutoka sekta za umma, binafsi, taasisi za kimataifa na wakulima wenyewe.
Tanzania nzima, na hususani miradi ya kipaumbele ya kilimo iliyo chini ya BRN, ilishuhudia uzalishaji mkubwa wa mahindi na mpunga katika msimu wa 2013/14; jambo ambalo limeleta fursa nzuri lakini pia lilikuja na changamoto zake. Kwa mfano katika msimu huo, uzalishaji wa mahindi ulifikia tani milioni 6 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani milioni 4.5 kwa wastani katika miaka mitano ya nyuma. Mpunga ulifikia tani milioni 1.7 kutoka tani milioni 0.85 mwaka uliotangulia.
Mwisho wa maabara hii, washiriki wataibua mapendekezo na mpango wa utekelezaji utakaoainisha mfumo madhubuti wa masoko ya mahindi na mpunga. Inatarajiwa kwamba mapendekezo haya yataweza kutumika kwa mazao mengine pia.    
Kwa maelezo zaidi, wasiliana na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Utetezi wa PDB:
Nyanda Shuli   Simu: +255 784600170           Baruapepe: nshuli@pdb.go.tz
Imetolewa Dar es Salaam na:
Omari Issa, Mtendaji Mkuu,
Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB)
                                                       ________________________

Kwa wahariri:
Kuhusu BRN
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa! (BRN) ni: Mfumo maalum wa utekelezaji wa miradi unaotumika kutekeleza Sekta Kuu za Kitaifa za Kipaumbele (NKRAs) kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa umma ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025, ya kuifanya Tanzania ifikie hadhi ya nchi yenye uchumi wa kiwango cha kati. Mfumo wa BRN unajumuisha mkakati wa utekelezaji, muundo wa usimamizi wa utekelezaji katika ngazi ya wizara na mipango mikakati. Kwa pamoja, mikakati hii inajenga mfumo wa maendeleo unaoweka vipaumbele katika ushirikishaji, uwazi na uwajibikaji.
Kuhusu Mfumo wa Maabara
Mfumo wa maabara katika BRN unahusisha kuwakusanya pamoja wataalamu na wadau wengine husika ili kufanya uchambuzi wa kina na kupata suluhu ya changamoto, kuainisha mikakati ya kipaumbele na kuainisha mpango wa kina wa utekelezaji wenye viashiria vinavyopimika.