Saturday 3 August 2013

Edward Mule Yesse awa huru baada ya kuwa katika kifungo cha al-Shabaab kwa miezi 18

Na Julius Kithuure, Nairobi

Hali nyumbani kwa Edward Mule Yesse katika eneo la makaazi la Buru Buru huko Nairobi ilikuwa ya machozi ya furaha, nyimbo za kusifu, kukumbatiana na karamu ya nyama choma.

Edward Mule Yesse (katikati), alipigwa picha akiwa na baba yake na mke wake, akiwasili nyumbani karibu na Nairobi baada ya miezi zaidi ya 18 ya kuwa kwenye kifungo cha al-Shabaab huko Somalia. [Julius Kithuure/Sabahi]

Mule, kama anavyojulikana na familia yake na marafiki zake, alitekwa tarehe 11 Januari, wakati wapiganaji wa al-Shabaab zaidi ya 100 walipofanya ghasia katika kambi ya Utawala ya Polisi huko Gerile, katika wilaya ya Wajiri kusini nchini Kenya, ambapo alipelekwa kama ofisa wa wilaya.

Mule, kwa sasa ana umri wa miaka 32, alitekwa pamoja na Fredrick Irungu Wainaina mwenye umri wa miaka 57, karani wa usajili kwenye wizara ya Uhamiaji na Usajili wa Watu.


"Tuliwekwa kwenye chumba kisicho na mwanga kwa kipindi chote hiki," Mule aliwaambia waandishi wa habari waliokusanyika nyumbani kwake Alhamisi (tarehe 1 Agosti). "Hakukuwa na anasa ya mwanga wa jua. 

Kwa kweli, macho yangu yanauma, yanakaza kwa sababu ya kuwekwa chumba chenye giza kabisa. Hata kuoga, tulioga kwenye giza nene, na kupokea simu zao, wahudumu wetu wa al-Shabaab walitufunika macho yetu na nguo nzito iliyokunjwa."

Mule (wa pili kutoka kushoto) akiungana tena na familia yake: baba Edward Yesse (kushoto), mkewe Mona (wa pili kutoka kulia) na mama Emma Yesse. [Na Julius Kithuure/Sabahi]

"Ingawaje al-Shabaab hawakututesa, walitutisha na kutuogofya," alisema, akiongezea kwamba al-Shabaab mara zote walitudhihaki kwa kifo. "Kwa kweli, mara moja walituvua nguo na kutuambia kuwa muda wetu wa kuchinjwa umewadia. Ilikuwa mpaka mabosi wao waingilia kati kusimamisha kipindi cha kutisha."


Mule alisema alipata malaria akiwa kifungoni, lakini al-Shabaab walimpatia matibabu. Alisema wanamgambo hao kwa kawaida huwapa wali na nyama kula lakini chakula kilikuwa hakitoshelezi.

Kuteswa kiakili ilikuwa si ya kuvumilika na kuteswa kimwili kwa kushikiliwa katika sehemu isiyo na mawasiliano ilikuwa jambo la kitia kihoro," Mule alisema.

Al-Shabaab waliwaachia Mule na Wainaina Jumanne baada ya majadiliano na serikali ya Kenya, mara baada ya familia za mateka kadhaa wa Kenya kutoa wito kwa serikali kuchukua hatua.

Mke wa Mule, Mona Garisse, familia yake pamoja na ndugu, marafiki na majirani wote walikusanyika kumkaribisha nyumbani.

Wakati akisubiri mwanaye wa kiume kurudi nyumbani Alhamisi, mama wa Mule Emma Yesse alipatwa na hisia kali. Uso wake ulighubikwa na machozi, mara chache akipata tabasamu wakati akiangalia picha ya mwanaye iliyokuwa kwenye fremu.

Sabahi ilikaa chini na baba wa Mule, Edward Yesse, kuzungumza juu ya mateso ya familia.

Sabahi: Je, unajisikiaje kuungana tena na mwanao?

Edward Yesse: Maneno hayawezi kuelezea furaha na faraja ninayohisi. Sikuweza kuepuka kulia wakati nilipomwona Mule. Nimefarijika na nina amani.

Sabahi: Hukuweza kumwona Mule hadi siku tatu baada ya kuachiwa kwake. Kwa nini hakuungana na familia yake mara tu baada ya kuachiwa kutoka kifungoni?

Yesse: Haikuwezekana kuja nyumbani moja kwa moja. Kulikuwa na taratibu za kufuatwa, kama vile usalama [kufanyiwa usaili] na kufanyiwa uchunguzi wa afya na kisaikolojia.

Sabahi: Je, ilikuwa vigumu kusubiri taratibu hizi baada ya kuwa na kuvumilia?

Yesse: Mule kwa sasa yuko hapa pamoja na sisi na hili ndilo lililo muhimu zaidi. Alisema alikuwa kwenye makao makuu ya Upelelezi wa Usalama wa Taifa mahali alipokuwa akisubiri taratibu za kufanyiwa usaili.

Sabahi: Ni lazima kwamba ulikuwa wakati mgumu kwa familia yako wakati Mule alipokuwa akishikiliwa mateka . Uliwezaje kukabili hali hii?

Yesse: Mke wangu, familia yangu na mimi tulikuwa tukisali mara nyingi. Tukimuomba Mungu kugusa nafsi za watekaji wasimdhuru kijana wangu.

Pia nilikuwa na shajara ambamo niliandika hatua zote ambazo mimi na serikali tulizichukua kumuokoa. Pia niliandika maneno yote niliyozungumza na watekaji na walichoniambia. Nitamuonyesha mtoto wangu maelezo haya katika shajara. Ni kumbukumbu ya kutia huzuni.

Sabahi: Sasa unajisikiaje?

Yesse: Sasa nina amani na furaha lakini nina wasiwasi kwa sababu kuna familia nyingine ambazo zina uchungu kwa sababu vijana wao ni mateka nchini Somalia. Moyo na mawazo yangu yanaenda kwa familia za wanajeshi waliotekwa na mashirika ya misaada. Ninawaomba al-Shabaab kuonyesha huruma na upendo kwa waliotekwa na kuwaachia bila ya masharti.

Sabahi: Je, ulilipa fidia yoyote kwa al-Shabaab?

Yesse: Ninataka kulieleza hili kwa uwazi: Familia yangu haikulipa hata senti, wala serikali ya Kenya. Ningeweza kupata wapi kiasi hicho kikubwa cha fedha? Kijana wangu na mtekwaji mwenzake, [Fredrick] Irungu Wainaina, waliachiwa bila ya malipo.

Sabahi: Lakini al-Shabaab walidai fidia ili kuwaachia.

Yesse: Ndiyo. Kwa hakika, walitoa madai ya fidia ya Dola 250,000. Hata hivyo, kiuhakika niliwaambia kwamba siwezi kupata hizo fedha. Miujiza hutokea na hatimaye Mungu aliwagusa watekaji.

Sabahi: Ni nani unayemshukuru kwa hatimaye kuachiwa kwa kijana wako?

Yesse: Ninamshukuru Rais wa Kenyat Uhuru Kenyatta, Makamu wake William Ruto, na idadi ya wazee wa ukoo wa Somalia wanaoheshimika. Pia naishukuru idara yetu ya upelelezi kwa kuwa na mawasiliano ya karibu na watekaji.

Sabahi: Ulichukua hatua gani baada ya al-Shabaab kutoa video ambapo walitishia kumuua Mule?

Yesse: Al-Shabaab ni kikundi cha waasi wenye siasa kali ambachohapo awali kimekuwa kikiwakata vichwa watu wasio na hatia. Wamewaua mamia kupitia ulipuaji wa mabomu na kupigwa risasi na ninahofia mabaya zaidi kutokea.

Wakati hatima ya mtu inapokuwa mikononi mwa kikundi hicho hatari, lolote linaweza kutokea. Ukweli kwamba al-Shabaab wamemuachia kijana wangu bila ya kumdhuru inaonyesha bado wana roho ya ubinadamu.

Sabahi: Nini ni ujumbe wako kwa al-Shabaab?

Yesse: Kwanza, ninawashukuru kwa kutomdhuru kijana wangu kwa namna yoyote. Ninawasihi kuacha vurugu nchini Somalia na kwingineko. Hakuna mafanikio yanayopatikana kupitia katika risasi, ugaidi na utekaji. Nina uhakika wanaweza kuweka silaha chini na kufuata jitihada zinazofanywa na serikali ya Somalia na jumuiya ya kimataifa kuleta amani na utulivu nchini Somalia.

Sabahi: Je, utamruhusu kijana wako kurudi kufanya kazi Wajir?

Yesse: Oh, ndiyo. Mule ni mtu mzima. Ni Mkenya mzalendo. Bahati nzuri, kama alivyosema waziri wa Mambo ya Ndani Ole Lenku, kijana wangu itabidi apate ushauri nasaha wa kina kabla ya kurejea kazini katika kituo cha kazi atakachochagua.

Sabahi: Ujumbe wowote kwa wazazi wa mateka wengine?

Yesse: Ndiyo. Wakati wowote kuna matumaini mwisho wa matatizo. Wazazi wenzangu katika hali ngumu kama hiyo wanapaswa kumwamini Mungu, kuomba faraja yake katika sala na kuamini kwamba serikali inajua mambo mazuri kwa ajili ya nchi. Wakati wote serikali ina maslahi mazuri kwa raia wake licha ya matatizo kama hayo.

Sabahi: Sasa wakati msukosuko huu umepita kwako, unapanga kusheherekea vipi?

Yesse: Ninaandaa karamu kubwa kwa ajili ya Mule wiki hii wakati wanafamilia wengine, ndugu na marafiki wanapofika kumuona.

Chanzo - sabahionline.com