Monday 26 November 2012









Leo Tarehe 26 Novemba 2012, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Peter Kallaghe amempokea na kumkaribisha Waziri wa Maji  Mhe. Jumanne Maghembe na ujumbe wake kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) katika Ofisi za Ubalozi hapa nchini Uingereza.  Mheshimiwa Maghembe na ujumbe wake uko nchini Uingereza kwa ziara rasmi ya kikazi na ya kiserikali. Ujumbe huo, ukiongozwa na Mhe. Maghembe, utapata fursa ya kutembelea Makampuni, Taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi zinazoshughulika na utoaji wa huduma ya Nishati  na Maji hapa Uingereza, vilevile Ujumbe huo utafanya majadiliano na Viongozi Wakuu katika Sekta hiyo ya Nishati na Maji kwa nia ya kupata ushauri wa Kitaalam wa kutafuta njia zaidi za kuboresha utoaji wa huduma hizo nchini kwetu Tanzania.

Mheshimiwa Balozi Kallaghe, alitumia fursa hiyo kumfahamisha Mhe. Waziri Maghembe maendeleo ya kazi za Diplomasia ambazo Ubalozi unafanya kwa niaba ya serikali nchini Uingereza.  Kwa upande wake Mheshimiwa Waziri Maghembe, alielezea mafanikio ya serikali katika kuwapatia wananchi huduma ya maji na juhudi zinazoendelea kufanywa kuondoa tatizo la Maji na kuhakikisha tatizo hilo linakuwa historia nchini Tanzania.

Waziri Maghembe anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na viongozi wakuu wa sekta ya Nishati na Maji nchini Uingereza yenye lengo la . Aidha ujumbe huo wa Tanzania, ukiongozwa na Mheshimiwa Waziri  Maghembe utamaliza ziara yake nchini Uingereza siku ya Alhamis, tarehe 29 Novemba 2012.

Mheshimiwa Waziri Maghembe, pamoja na Mheshimiwa Balozi Kallaghe, wakiwa kwenye picha ya pamoja na Ujumbe wa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na baadhi ya Maofisa wa Ubalozi hapa London.